Thursday, March 12, 2009

NGUVU YA UMOJA

NGUVU YA UMOJA
MWANZO 11;1-9 Nchi yote ilikuwa na lugha moja na usemi mmoja.Ikawa watu waliposafiri waliona nchi tambarare katika nchi ya shinari wakakaa huko………………4,Wakasema haya na tujijengee mji ,na mnara,na kilele chake kifike mbinguni,tujifanyie jina ilitusipate kutawanyika usoni pa nchi yote.Bwana akashuka ili auone mji na mnara waliokuwa wakiujenga wanadamu.Bwana akasema tazama watu hawa ni taifa moja,na lugha yao ni moja,na haya ndio wanayoanza kuyafanya wala sasa hawatazuiliwa neno wanalokusudia kulifanya.Haya na tushuke huko tuwachafulie usemi wao ili wasisikilizane wao kwa wao……………………
Neno umoja lina maana ya kupatana,kuafikiana,kuelewana na mwingine,pia ni hali ya kulingana katika roho,katika nia,katika mawazo,katika maneno na matendo yao.

Baada tu ya gharika ya nuhu kile kizazi kilichopona au kisichoangamizwa kiliendelea kuishi.Watu hawa walishi wakiwa na lugha moja na usemi mmoja.

Lugha moja ni hali ya watu wa eneo Fulani kusikilizana wanapozungumza na hivyo kufanya wawasiliane,hii haijalishi kama wana mahusiano mazuri au hapana.

Usemi mmoja ni hali ya watu kuelewana, kuafikiana,kupatana na hivyo kulingana katika jambo wanalopanga katika nia zao,katika mawazo yao na katika maneno na matendo.

Watu hawa walipanga kujenga mnara ambao ungefika mbinguni na shida ilikuwa kujijengea mnara wao wenyewe na kwa utukufu wao wenyewe si kwa utukufu wa Mungu.

Mambo manne ambayo yanaelezea nguvu ya umoja katika aya hii;
1.Msitari wa 3-4.kujishughulisha na lengo.
Mara zote panatakiwa kutazama lengo,watu wanapokuwa katika umoja au shirika au jumuia au kanisa.Ili mafanikio yaonekane panatakiwa watu walio kwenye umoja waangalie sana lengo.Bila ya kutazama lengo hakuna mafanikio yoyote yatakayotokea.

2.Msitari wa 6;umoja kutawala katika jumuia au watu.
Kama tulivyokwisha eleza hapo juu kwamba panatakiwa kuingiliana kitabia ili pawe na matokeo mazuri.Nikichukua mfano wa ndoa,panatakiwa sana umoja ili pawepo na matokeo mazuri juu ya ndoa husika.Wanandoa wengi hawazioni baraka za Mungu kwa sababu ya magomvi,matusi,kutoka nje ya ndoa,hata wivu wa kimapenzi,mume anapanda kwenye mti mke akienda sokoni,iliaone anaongea na nani njiani.Ndugu sahau kabisa kuwa kuna kubarikiwa unapokuwa na tabia zilizoko hapo juu.







3.Msitari wa 1,6;mawasiliano mazuri katika kikundi au jumuia.
Mawasiliano ni kitu muhimu sana kwenye jumuiya au ndoa.Mawasiliano mara zote yanahusisha pande mbili ambazo ziko katika umbali Fulani.Mawasiliano yanaweza kufanyika kwa njia ya mdomo,simu,email hata kwa barua.Nakumbuka wanandoa ambao walikuwa wanawasiliana kwa barua ndani ya nyumba.Siku moja baba mwenye nyumba aliandika kimeseji kuwa anapumzika na hivyo mke wake amuamshe wakati wa kwenda kazini.Mama alipokiona kile kimeseji naye akaandika muda umefika wa kwenda kazini.Baba alipoamka na kukuta kimeseji akajifunza kuwa hayo hayakuwa mawasiliano,toka siku hiyo akaanza kuongea na mkewe.Kikundi kinatakiwa kuboresha mawasiliano mara zote ili mafanikio ya kila siku yaonekane.Nikiwa kama mratibu wa shirika lisilo la kiserikali,nilijifunza sana umuhimu wa mawasiliano.Kwanza mawasiliano na Mungu,na walioko juu yangu na walioko chini yangu.Mahali ambapo nilizembea kidogo tu kufanya mawasiliano matokeo yake hayakuwa mazuri.Mungu alichafua mawasiliano ya wale watu ili wasitimize lengo walilojiwekea.

4.Msitari wa 7-9; kufanya mapenzi ya Mungu.
Mapenzi ya Mungu ni hali ya kufanya jambo linalompendeza Mungu na linalompa Mungu utukufu.Katika mistari hii tunaona namna ambavyo watu walijenga mnara ambavyo walishindwa kufanya mapenzi ya Mungu lakini walitamani kufanya mapenzi yao pale waliposema,na tujijengee mnara utakaofika mbinguni ili tujifanyie jina.Hawakutaka kuliinua jina la Bwana bali kuliinua jina lao wenyewe.




ZABURI 133;1 Tazama ilivyo vema na kupendeza ndugu wakae pamoja kwa umoja.Ni kama mafuta mazuri kichwani,yashukayo ndevuni,ndevu za Haruni,yashukayo mpaka upindo wa mavazi yake.Kama umande wa Hermoni,ushukao milimani pa sayuni,maana ndiko Bwana alikoamuru baraka,Naam uzima hata milele.

Hii ni zaburi ndogo kuliko zote lakini yenye utajiri mkubwa.Yako mambo kadhaa tunayoweza kujifunza hapa ambayo watu wakizingatia watafanikiwa sana;
i.kukaa pamoja na kwa umoja,ni hali ya kuelewana kwa watu waliopamoja kwa dhati bila unafiki.
ii.mafuta mazuri kichwani,ni roho mtakatifu au upako au msaada anaoupata mtu anapojazwa roho bora ya Mungu.Upako unatakiwa uwe msaada katika maeneo yote ya mtu aliyeokoka kiroho,kimwili,kijamii hata kiuchumi.
iii.umande wa Hermoni,ni mfano wa baraka za Mungu zinashuka kwa watu wa Mungu.Mara zote watu wasiookoka wanapokuwa na pesa,watu husema wamebarikiwa.Lakini baraka za kweli zinatoka kwa Mungu na hivyo watu waliookoka peke yao ndio wanao barikiwa.Watu wasiookoka wana mbinu nyingi za kiibilisi za kuwafanikisha lakini hawana amani,ndoa zao hazina amani,hofu imewajaa.